Headline

YANGA IMETWAA TUZO NNE LIGI KUU TANZANIA BARA

Yanga usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kubeba tuzo nne katika utoaji wa zawadi za waliofanya vizuri kwenye msimu uliopita wa Ligi ya Vodacom Tanzania
Licha ya ubingwa wa taji la Vodacom pia beki Juma Abdul ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu wa 2015/2016, kwa kumbwaga Mohamed Hussein wa Simba na kiungo wa Mtibwa Sugar Shizza Kichuya.
Mbali na tuzo hiyo, Abdul atajinyakulia kitita cha fedha Sh Milioni 9.2 na hiyo kuwa tuzo yake ya pili kwa msimu uliopita baada ya ile ya mchezaji bora wa mwezi Machi 2016.

Tuzo nyingine ambayo imekwenda Yanga ni ile ya mfungaji bora ambayo imechukuliwa na Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21 na kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7. wakati kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe Thabani Michael Kamusoko anayechezea Yanga pia akishinda tuzo ya  mchezaji bora wa kigeni, na kujinyakulia kitita cha Sh. Milioni 5.7.


Kocha Mdachi Hans van der Pluijm aliiongezea Yanga tuzo ya nne kwa kuibuka kocha bora wa msimu uliopita na kujinyakulia Sh. Milioni 8.

Na zawadi ya tano ambayo ilikuwa inaongozwa kwa ukubwa katika tuzo zote zilizotolewa na Vodacom ilikuwa ni ile ya ubingwa ambayo ilichukuliwa na Yanga na kujizolea Sh. Milioni 81.3 kwa kuwa bingwa, huku Sh. Milioni 40.6 zikienda kwa washindi wa pili, Azam FC, Sh Milioni 29 zikienda kwa washindi wa tatu, Simba SC na Sh. Milioni 23.2 zikienda kwa Prisons washindi wa nne.
Katika tuzo hizo kipa wa Azam FC, Aishi Salum Manula ameshinda tuzo ya kipa Bora akiwaangusha Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Benno Kakolanya wa Prisons.
Mshambuliaji wa Simba Ibrahim Hajib aliibuka mshindi wa tuzo ya goli bora la msimu na kuzawadiwa Sh. Milioni 3 akimuangusha Tambwe wa Yanga, wakati Mtibwa Sugar imeibuka timu yenye nidhamu bora na kuzishinda timu za JKT Ruvu na Mgambo Shooting na kuzawadiwa Sh. Milioni 17.2.
Ngole Mwangole ameshinda tuzo ya Refa Bora na kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7 baada ya kuwaangusha Anthony Kayombo na Rajab Mrope.

Chanzo@Goal.com



No comments